Watu 6 wamefariki dunia kwa mmomonyoko Ufilipino

Serekali ya kusini mwa Ufilipino inasema watu 6 wamefariki dunia na wengine kadhaa hawajulikani walipo baada ya kutokea mmomonyoko wa ardhi katika kijiji cha uchimbaji wa dhahabu.

Maafa hayo yametokea Jumanne usiku kijijini Masara, katika mji wa Maco, wa jimbo la Davao de Oro.

Mmomonyoko huo wa udongo umeharibu nyumba kadhaa na kufukia mabasi mawili yaliyokuwa yakitumika kuwasafirisha wafanyakazi mpaka kwenye mgodi huo unaoendeshwa na kampuni ya Apex Mining yenye makao ya Ufilipino.

Msemaji wa serikali ya mkoa anasema kikosi cha uokozi kinachimba vifusi ili kuwapata wachimba 27 waliokuwa kwenye mabasi hayo mawili wakati mmomonyoko wa ardhi unatokea.

Wachimba migodi wengine wanane walijiokoa kwa kuruka madirishani kabla ya mabasi hayo kufukiwa matope.

Amesema watu 46 wamepotea, ingawa idadi hiyo ikijumuisha wachimbaji 27.