Watu 52 wauawa katika mapigano eneo la mpakani kati ya Sudan na Sudan Kusini

Ramani ya Sudan Kusini

Zaidi ya watu 50 wakiwemo wanawake na watoto, waliuawa kwenye eneo la mpaka kati ya Sudan Kusini na Sudan, afisa wa eneo hilo amesema Jumatatu.

Ni tukio baya la mauaji tangu mwaka wa 2021 katika msururu wa mashambulizi yanayohusiana na mzozo wa mpaka.

Vijana wenye silaha kutoka jimbo la Sudan Kusini la Warrap walifanya mashambulizi ndani ya jimbo jirani la Abyei, waziri wa habari wa Abyei Bulls Koch amesema.

Abyei ni eneo lenye utajiri wa mafuta ambalo linatawaliwa kwa pamoja na Sudan Kusini na Sudan, ambazo zote zinadai ni eneo lao.

Koch ameiambia Reuters kwamba watu 52, kati yao wanawake, watoto na maafisa wa polisi, waliuawa wakati wa mashambulizi siku ya Jumamosi. Wengine 64 walijeruhiwa.