Mapigano makali kati ya makundi hasimu huko Darfur nchini Sudan yameua watu 45, maafisa wamesema Alhamisi, huku viongozi wa kikabila wakiripoti kwamba mapigano yaliendelea katika ghasia za kikabila za hivi karibuni.
Mapigano mapya yalizuka Jumanne kati ya Waafrika wa kabila la Fallata na kabila la Waarabu katika vijiji vilivyoko nje ya Nyala, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kusini, mashahidi walisema.
“Watu 15 waliuawa katika mapigano kati ya kabila la Fallata na Rizeigat Jumanne, na 30 waliuawa Jumatano,” kamati ya usalama ya jimbo la Darfur Kusini imesema katika taarifa.
Kamati hiyo imeongeza kuwa, wanawake na watoto ni miongoni mwa waliouawa katika mapigano.
Awali, viongozi wa kabila la Fallata na Rizeigat waliiambia AFP kwamba mapigano yalikuwa yakiendelea hadi Alhamisi.