Maandamano hayo ni ya kushinikiza kujiuzulu kwa waziri mkuu Sheikh Hasina, na yalianza mapema mwezi uliopita, pale wanafunzi wa vyuo vikuu walipoanza kuitisha kuondolewa kwa sheria kandamizi kwenye ajira za serikali, na kupelekea ghasia ambazo zimeuwa zaidi ya watu 200 kufikia sasa.
Kufuatia hali hiyo serikali ilifunga shule zote pamoja na vyuo vikuu nchini, huku ikisitisha huduma za internet, pamoja na kuweka sheria ya kutotoka nje nyakati za usiku. Kufikia sasa takriban watu 11,000 wamekamatwa na polisi.
Waandamanaji wamekuwa wakiomba wananchi kukaidi mamlaka, kususia kulipa kodi, pamoja na kutokwenda kazini Jumapili, ambayo ni siku ya kufanya kazi nchini Bangladesh. Ofisi, benki, pamoja na viwanda kwenye mji mkuu wa Dhaka zimefunguliwa Jumapili, lakini wafanyakazi wengi walitatizika kutokana na uhaba wa huduma za usafiri.
Ripoti zimeongeza kusema kuwa waandamanaji wameshambulia chuo kikuu cha matibabu cha Sheikh Mujib, mjini humo, huku wakiteketeza magari kadhaa.