Watu 179 wathibitishwa kupoteza maisha kwa ajali ya ndege Korea Kusini

Eneo la ajali ya ndege, Muan, Korea Kusini.

Serekali ya Korea Kusini imesema takriban watu 179 wamefariki dunia baada ya ndege ya abiria kuungua Jumapili iliposerereka kwenye njia ya kurukia na kutua  ndege na kugonga uzio wa zege.

Ripoti za awali zinaonyesha matairi ya ndege yalishindwa kutoka wakati ndege ya Jeju Air ilipokuwa ikitua Muan, takriban kilomita 290 kusini mwa Seoul.

Ndege hiyo iliyobeba watu 181 ilikuwa ikirejea kutoka Bangkok. Ni moja ya maafa mabaya zaidi katika sekta ya anga ya Korea Kusini.

Kati ya watu 179 waliokufa, 65 wametambuliwa, limesema shirika la zima moto la Korea Kusini.

Watu wawili wote wakiwa ni wafanyakazi, walitolewa nje ya mabaki ya ndege wakiwa hai.

Picha za video zilizorushwa na televisheni ya Korea Kusini zinaonyesha ndege hiyo aina ya Boeing 737-800 ikipita kwa kasi katika njia baada ya kutua na kugonga kizuizi cha zege na kusababisha mlipuko mkubwa.

Magari kadhaa ya zima moto yalipelekwa eneo la tukio kujaribu kuzima moto huo.