Zaidi ya wiki mbili za mapigano kati ya jeshi la Sudan na kundi la wanamgambo kwenye mji mkubwa katika mkoa wa Darfur magharibi, yamesababisha vifo vya watu 123, limesema Jumapili shirika la kimataifa la misaada.
Mapigano katika mji wa el-Fasher, mji mkuu wa jimbo la North Darfur, pia yaliwajeruhi zaidi ya watu 930 katika kipindi hicho hicho, shirika la madaktari wasio na mipaka limesema.
Hii ni ishara ya kuongezeka kwa mapigano, kundi hilo lilisema. Tunatoa wito kwa pande zinazohasimiana kuchukua hatua zaidi kuwalinda raia. Mapigano kati ya jeshi na vikosi vya wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF) yaliongezeka mapema mwezi huu katika mji huo, na kuwalazimisha maelfu ya watu kuyakimbia makaazi yao, kulingana na Umoja wa Mataifa.
El-Fasher imekuwa kitovu cha mgogoro kati ya jeshi na RSF, ambayo inasaidiwa na wanamgambo wa Kiarabu wanaojulikana kama Janjaweed. Mji huo ni ngome ya mwisho ambayo bado inashikiliwa na jeshi katika jimbo la Darfur.