Watu 11 wauawa na waasi wanaoshukiwa kuwa ni wa kundi la ADF mashariki mwa DRC

Wanajeshi wa Uganda waonekana kwenye barabara ya Mbau-Kamango katika wilaya ya Beni jimbo la Ituri, Disemba 8, 2021, ambako kuna ngome za waasi wa ADF.

Wanavijiji 11 waliuawa katika mashambulizi yaliyotekelezwa na waasi wanaoshukiwa kuwa ni wa kundi la ADF mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, maafisa wa eneo hilo wamesema Jumanne.

Kundi la Allied Democratic Forces, lenye uhusiano na kundi la Islamic State, Jumatatu lilifanya mashambulizi katika vijiji kadhaa katika Wilaya ya Mambasa kwenye jimbo la Ituri, maafisa hao wamesema.

Matadi Muyapandi, afisa wa polisi katika wilaya ya Mambasa, amesema miili 11 ilipatikana katika “maeneo tofauti ya msitu”.

Jeshi lilikuwa linawasaka waasi katika wilaya ya Irumu huko Ituri, na wilaya ya Beni katika jimbo jirani la Kivu Kaskazini, amesema.

Mandela Moise, mkuu wa shirika la kiraia huko Babila Babombi katika wilaya ya Mambasa, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba watu 13 waliuawa, wengi wao walikuwa wakulima.