Mafuriko yauwa watu 10 Tanzania

Mafuriko yaliyotokea mjini Dar es Salaam, Tanzania, Disemba 21, 2011.

Watu 10 wamepoteza maisha kutokana na mafuriko mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania, Mkuu wa Mkoa Paul Makonda amesema.

“Tunaendelea kupokea taarifa kwa sababu tunawataalamu wetu katika kila kata,” ameongeza Makonda.

Ameeleza kuwa Jeshi la kuzima moto, kitengo cha huduma ya haraka, Jeshi la polisi wanaendelea kupokea taarifa kutoka maeneo mbalimbali.

Makonda amewarai wananchi walioko katika maeneo salama ni vyema wakatulia majumbani katika kipindi hiki kwani utabiri wa hali ya hewa unaonyesha mvua zitaendelea Jumatatu na Jumanne.

Pia amewatahadharisha wale walioko katika maeneo hatarishi akisema: “Ningewaomba waende maeneo ambayo wanaweza kuwa salama, wakati tunatafuta utaratibu mzima wa namna gani tunaweza kupunguza kero. Hususan Changamoto ya maji kutopita katika mitaro."

Vyanzo vya habari mjini Dar es Salaam vimeripoti kuwa usafiri wa mabasi ya mwendokasi umesitishwa kutokana na mafuriko eneo la Jangwani.

Sababu iliyopelekea mabasi hayo kusitisha safari zake ni kufurika maji njia za mabasi hayo na vituo vilivyoko katika njia hiyo.