Watoto wa Rohingya wazama wakikimbia mauaji Myanmar

Mkimbizi wa Rohingya aliyevuka mpaka kuingia Bangladesh akiwa anatayarisha makazi ya muda katika kambi ya wakimbizi

Polisi nchini Bangladesh wanasema watu watano wamezama, wanne kati yao ni watoto, na wengine wengi hawajulikani walipo.

Ajali hiyo imetokea baada ya boti lililokuwa na Waisalmu wa Rohingya 50 kutoka jimbo la Myanmar la Rakhine, walipokuwa wakielekea Bangladesh kwa kutumia mto Naf.

Serikali ya Bangladesh inasema kwamba waokoaji wameopoa miili ya mwanamke mmoja na watoto wanne katika eneo la tukio mapema Jumatatu.

Maafisa wa Bangladesh wanasema watu 21 wamesalimika katika ajali hiyo.

Vyanzo vya habari nchini Bangladesh vimeripoti kuwa zaidi ya Wa-Rohingya nusu milioni wameshavuka mpaka kuingia nchi ya jirani Bangladesh katika wiki za hivi karibuni.

Watu hao wanakimbia ili kujinusuru kutokana na mashambulizi yanayofanywa na jeshi la Burma, baada ya wanamgambo wa Rohingya kufanya mashambulizi kwa vikosi vya serekali.