Watoto 30,000 wakoseshwa makazi Msumbiji ndani ya mwezi mmoja

Familia iliyotoroka nyumbani ikihofia usalama Msumbiji

Wimbi jipya la ghasia katika eneo la kaskazini mwa Msumbiji, linaloendelea kukumbwa na mashambulizi ya wanajihadi, liliwafurusha takriban watoto 30,000 mwezi Juni, 2022, ripoti mpya inaonyesha.

Hii ndiyo idadi kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa katika mwezi mmoja, kwenye mgogoro huo wa muda mrefu, shirika la misaada la Uingereza liliripoti jumaa.

Juni ilishuhudia mashambulizi mengi katika jimbo la Cabo Delgado, ambapo wanajihadi walianzisha uasi wa umwagaji damu mwaka 2017, uliopelekea kutumwa kwa ujumbe wa kijeshi wa kikanda mwaka jana, ambao ulikuwa umerejesha hali ya usalama.

Takriban watu 53 waliuawa katika wilaya kadhaa, na kuwalazimu zaidi ya watu wazima na watoto 50,000 kukimbia makwao, shirika la misaada la Save the Children lilisema.

"Huu umekuwa mwezi mbaya zaidi kwa familia na watoto huko Cabo Delgado katika mwaka huu," Brechtje van Lith, mkurugenzi wa shirika hilo nchini Msumbiji, alisema katika taarifa. Alisema wengi wa watu wanaokimbia ghasia, ambao wamefikia zaidi ya 700,000, walikuwa hawana makazi.

Takriban watu 4,100 wameuawa nchini Msumbiji tangu mwaka 2017, kwa mujibu wa shirika linalofuatilia mizozo la ACLED.

Wanajeshi 3,100 kutoka nchi kadhaa za Kiafrika walitumwa huko Cabo Delgado Juni mwaka jana na kuchukua tena udhibiti wa eneo kubwa.