Watatu wauwawa katika maandamano ya Senegal

Idadi ya watu waliouwawa katika maandamano nchini Senegal kutokana na kuahirishwa kwa uchaguzi wa rais mpaka Desemba imeongezeka mpaka kufikia watu watatu, huku wasiwasi ukiongezeka kwamba moja ya demokrasia iliyosalia katika ukanda wa mapinduzi wa Afrika Magharibi ipo hatarini.

Tangazo la kucheleweshwa kwa uchaguzi huo wiki tatu tu kabla ya upigaji kura uliopangwa wa Februari 25 lilizusha makabiliano makali siku ya Ijumaa kati ya waandamanaji na polisi mjini Dakar na miji mingine kadhaa, katika wimbi la machafuko ambayo wengi wanahofia yatasambaa na kusababisha kukosekana kwa utulivu kwa muda mrefu.

Rais Macky Sall amesema ucheleweshaji huo ni muhimu kwa sababu mizozo ya uchaguzi ilitishia uaminifu wa uchaguzi, lakini baadhi ya wabunge wa upinzani wameshutumu hatua hiyo na kusema ni mapinduzi ya kitaasisi.