Watu watatu walifariki dunia na wengine wanane kujeruhiwa wakati helikopta iliyokuwa ikiendeshwa na kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia ilipoanguka Jumamosi katika mkoa wa Lower Shabelle nchini humo, taarifa ya kikosi hicho ilisema jana Jumapili.
Katika taarifa hiyo Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) kilisema helikopta hiyo, iliyokuwa na abiria kumi na moja wakiwemo wanajeshi kutoka jeshi la Somalia, ilikuwa katika mazoezi ya kuwaokoa majeruhi wakati ajali hiyo ilipotokea.
“Tunasikitika abiria watatu kati ya abiria kumi na mmoja waliokuwemo ndani ya helikopta hiyo walipoteza maisha. Maafisa wanane waliojeruhiwa wamehamishiwa Mogadishu kwa matibabu ya haraka,” ATMIS ilisema katika taarifa hiyo.