“Watapata wanachotafuta, watajuta sana, NRM ndio wataalam wa vurugu,” aonya Museveni

Mfuasi wa Bobi Wine akikamatwa na polisi Nov 18 2020

Rais wa Uganda Yoweri Museveni ameonya wafuasi wa upinzani wanaoandamana kwa siku ya pili mfululizo katika sehemu  mbalimbali nchini humo, baada ya polisi kumkamata mgombea  urais Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine, akisema kwamba wanaoandamana “watakipata wanachotafuta.”

“mtajuta sana” ameonya Museveni wakati anafanya kampeni yake anayoiita ya kisayansi, Kaskazini mwa Uganda ambapo anaendelea kukutana na viongozi wa juu wa chama chake cha National resistance movement - NRM.

“Wale ambao wanaandamana wakishambulia wafuasi wa chama cha NRM jijini Kampala watapoteza hamu hivi karibuni kwa kiasi kwamba hata wataogopa kugusa fulana ya chama cha NRM hata kama imetupwa kando mwa barabara. Wameanza vita ambavyo tunajua vizuri sana.” amesema Museveni.

Maandamano yalifanyika sehemu mbalimbali nchini Uganda Jumatano na yameendelea kwa siku ya pili, baada ya polisi kumkamata mgombea wa urais Bobi Wine katika wilaya ya Luuka, mashariki mwa Uganda.

Polisi walitumia maji ya kuwasha, gesi ya kutoa machozi na risasi za moto kukabiliana na waandamanaji. Taarifa ya polisi imesema kwamba watu 16 wameuawa na 65 kujeruhiwa lakini baadhi ya vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kwamba huenda idadi ya waliouawa ni zaidi ya hiyo.

zaidi ya watu 300 wamekamatwa.

Museveni amesema kwamba chama cha NRM kina wataalam wa fujo.

“Mmeamua kupigana na NRM wakati sisi ndio wataalam wa vita. Mtajuta sana,” amesema Museveni akiongezea kwamba “najua biblia inasema kwamba mtu akikupiga kofi upande mmoja, unageuza upande mwingine ili akupige. Mimi huwa nafanya mambo kinyume. Yesu alipopata watu wamegeuza nyumba ya baba yake na kuifanya soko, alizua vurugu san ana hakuna mahali imeandikwa kwamba alilipa fidia.”

Museveni amedai kwamba waandamanaji wanaungwa mkono na nchi za nje, ambazo hazitaki kuona maendeleo Uganda. Hakutaja nchi hizo wala kudhibithisha madai yake.

“watapata wanachotafuta. Hawatatupambaza. Watajuta kabisa.” Rais Museveni ameendelea kurudia maneno hayo.

Viongozi wa dini wataka Bobi Wine kuachiliwa huru

Muungano wa viongozi wa dini kote Uganda umekemea vitendo vya fujo na mauaji ambayo yametokea baada ya Bobi Wine kukamatwa na kutaka mwanasiasa huyo kuachiliwa huru haraka iwezekanavyo.

Katika kikao na waandishi wa habari jijini Kampala, mwenyekiti wa muungano huo Sheikh Shaban Mubajje ameomba serikali kumwachilia mwanasiasa huyo haraka iwezekanavyo ili kurejesha hali ya amani na utulivu.

Anataka pia wafuasi wake waliokamatwa wakati wa maandamano kuachiliwa huru.

Muungano huo umeeleza wasiwasi kwamba hali ya kisiasa ilivyo sasa nchini Uganda inaweka mazingira magumu ya kufanyika uchaguzi ulio huru na haki.

“Tunaelewa hali ngumu wanayokumbana nayo maafisa wa usalama, lakini tunataka waheshimu uhai wa binadamu. Wanastahili kufanya kazi yao kwa uadilifu bila kuzingatia vyama vya kisiasa.” Amesema Mubajje.

“Jeshi limevunja ibara ya 209 ya sheria inayosema kwamba wanajeshi wa Uganda wanastahili kushirikiana na raia wakati kuna hali ya dharura na majanga kama la Covid-19.” Imesema taarifa ya baraza la viongozi wa kidini.

Taarfia hiyo inaendelea kusema kwamba “japo polisi wanadai kwamba wanatekeleza masharti ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya Corona, tumeona wazi kwamba na wao wanavunja masharti hayo. Wamevunja pia ibara ya 21 (3) ya sheria, inayosema kwamba polisi wanastahili kuwa wazalendo na kutenda kazi yao kwa uadilifu.”

Jeshi lasisitiza linafanya kazi ipasavyo

Msemaji wa jeshi la Uganda UPDF Brig Flavia Byekwaso, amewaambia waandishi wa habari kwamba wanajeshi wanaendelea kufanya kazi kulingana na sheria na wanatumia nguvu pale inapostahili ili kuondoa hatari inayoweza kuletwa na waandamanaji.

Amesema kwamba wanajeshi ambao wamerekodiwa wakiwapiga watu risasi za moto, wamefanya hivyo katika hatua ya kujilinda, akiongezea kwamba “waliowapiga watu risasi kiholela watachukuliwa hatua baada ya uchunguzi kufanyika.”

Tume ya uchaguzi atishia kuwaondoa baadhi ya wagombea

Wakati huo huo, tume ya uchaguzi imesema kwamba itawaondoa wagombea wanaokosa kufuata masharti yaliyowekwa kuzuia kusambaa kwa virusi vya Corona wkaati wa kampeni.

“Tume ya uchaguzi inawaonya wagombea wote wanaoendelea kukiuka masharti kwamba majina yao yatafutwa kutoka kwa orodha ya wagombea.” Amesema mwenyekiti wa tume hiyo Jaji Simon Byabakama katika taarifa kwa vyombo vya habari.

“Tunaisitiza kwamba wagombea wanaoendelea kuwakusanya watu katika mikutano yao ya kampeni, wakikiuka maagizo ya afya kulingana na sheria namba 3 iliyotolewa Novemba 19, 2020 wataondolewa kwenye orodha ya wagombea.” Imesema taarifa ya tume ya uchaguzi.

Kulingana na tume ya uchaguzi, mkutano wa kampeni haustahili kuhudhuriwa na zaidi ya watu 200.

Wagombea wengine wasitisha kampeni kutaka Bobi Wine aachiliwe

Baadhi ya wagombea wa urais kama Jenerali Mugisha Muntu, ambaye alikuwa mkuu wa jeshi, na Jenerali Henry Tumukunde, ambaye alikuwa waziri wa usalama, wamesitisha kampeni zao hadi Bobi Wine atakapoachiliwa huru.

Wagombea wa upinzani wanaishutumu serikali na tume ya uchaguzi kwa upendeleo.

Mwanamuziki Moses Saali, maarufu kama Bebe cool, anaendelea kuvutia umati mkubwa wa wafuasi wa chama cha Museveni NRM, akimfanyia kampeni, bila kuzuiliwa na polisi.

Maelfu ya wafuasi wa NRM wamekuwa wakiandaa mikutano mikubwa kaskazini mwa Uganda inayoongozwa na Bebe Cool.

Tume ya uchaguzi, polisi, Museveni, wala jeshi halijazungumzia hatua ya Bebe cool kuvutia umati mkubwa wa watu katika kampeni bila kuzuiliwa.

Bebe cool alitangaza kwamba amepewa ruhusa na Museveni kukabiliana kwa kila hali na mwanamuziki mwenzake, Bobi Wine.

Umoja wa mataifa unafuatilia hali Uganda

Ofisi ya katibu mkuu wa Umoja wa mataifa imesema kwamba inafuatilia kwa karibu sana yanayoendelea Uganda.

Taarifa iliyowekwa kwenye wavuti wa umoja wa mataifa inamnukuu msemaji wa katibu mkuu Stephane Dujarric, akisema kwamba “ni muhimu kwa taasisi za serikali hasa maafisa wa usalama kuheshimu haki za kibinadamu na sheria ili kuweka mazingira sawa kwa wagombea wote wa kisiasa. Tutaendelea kufuatilia kwa karibu sana yanayoendelea nchini humo n ani muhimu kwa wanasiasa wote na viongozi serikali kuhakikisha kwamba uchaguzi wa nchi hiyo unakuwa wa amani.”

Stephane amesema kwamba “kila mtu ana haki ya kufanya maandamano kwa amani na matumizi ya nguvu na maafisa wa usalama ni jambo ambalo linatia wasiwasi.”

Umoja wa ulaya umesema kwamba hautatuma waangalizi kufuatilia uchaguzi mkuu wa Uganda mwaka ujao 2021 kwa sababu mapendekezo yake 30 ya mwaka 2016 ambayo yalitakiwa kutekelezwa ili kuhakikisha uchaguzi huru na haki, yalipuuzwa kabisa na hakuna hata moja limetekelezwa kuelekea uchaguzi wa mwaka 2021.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC