Wasiwasi waongezeka kuhusu hali ya Venezuela

  • VOA News

Waandamanaji nchini Venezuela wakipinga matokeo ya uchaguzi ambapo serikali yadaiwa kufanya ukamataji holela wa wapinzani.

Maoni kutoka maeneo mbalimbali ulimwenguni yameonyesha wasiwasi Jumapili juu ya kuongezeka kwa idadi ya watu wanaokamatwa nchini Venezuela kufuatia uchaguzi wa mwishoni mwa wiki iliyopita.

Papa Francis, amesema Venezuela inapitia hali mbaya alipotoa ujumbe wake wa kila Jumapili, Vatican, na kuongeza kutoa mwito kwa pande zote kutafuta suluhu ili kuepuka kila aina ya ghasia.

Matamshi hayo yametolewa saa chache baada ya Rais wa Venezuela Nicolas Maduro, Jumamosi kutangaza kwamba serikali imewakamata wapinzani 2,000.

Katika mkutano wa hadhara katika mji mkuu wa Venezuela, Caracas, Maduro aliahidi kuwashikilia watu zaidi na kuwapeleka gerezani.

Naibu mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani, Jon Finel, akiongea na CBS, Jumapili amesema utawala wa rais wa Marekani, Biden, una wasiwasi na kamata-kamata ya Venezuela.