Wasiwasi kuhusu usafishaji wa kiwanda cha nyuklia, Japan

Waziri mkuu mpya wa Japan Fumio Kishida.

Waziri mkuu mpya wa Japan Fumio Kishida amesema Jumapili kwamba mpango wa kuondoa maji taka yaliyoko kwenye kiwanda cha nyuklia kilichoharibiwa na tsunami cha Fukushima utaendelea kama ilivyopangwa licha ya wasiwasi wa kimazingira kutoka kwa wakazi wanaoishi karibu.

Akizungumza wakati wa ziara yake ya kwanza kwenye kiwanda hicho tangu kuchukua madaraka,Kishida amesema kwamba serikali yake itafanya kila jihudi kuhakikisha usalama wa wakazi wakati wa shughuli hiyo ya usafishaji.

Kiwanda hicho kiliharibiwa vibaya kufuatia tetemeko la ardhi pamoja na tsunami iliyotokea mwaka wa 2011. Serikali ikishirikiana na kampuni ya kitaifa ya kusambaza umeme ya TEPCO, Aprili ilitangaza mpango wa kuanza kuondoa maji taka yaliyoko kwenye kiwanda hicho na kisha kuyamwaga kwenye bahari ya Pacific kuanzia mwaka wa 2023.

Mpango huo hata hivyo umepingwa vikali na wavuvi, wakazi wa Japan pamoja na wale kutoka China na Korea Kusini. Baadhi ya wanaopinga wanahofia kwamba maji hayo huenda yakawa na chembechembe za nyuklia ambazo ni hatari kwa maisha ya wanadamu, samaki na mimea.