RAILA odinga ni miongoni mwa wanasiasa maarufu sana nchini Kenya na ambao wamekuwa katika siasa za nchi hiyo kwa miaka mingi. Ana umaarufu wa jina na ameshika nafasi mbali mbali katika serikali ya Kenya.
Kwa wengi Raila Odinga anaonekana kuwa mtu ambaye amekuwa akigombania urais maisha yake yote. Lakini kwa hakika hakuna maoni yanayokubaliana katika kumwelezea mwanasiasa huyo – kuna wanaomuona kuwa mtu anayesukumwa na kiu kubwa ya kuwa rais, na wengine wanamwona kuwa mwanasiasa hodari aliyefanikiwa kudumu katika siasa za Kenya kwa muda wote huu.
Marafiki na hata wapinzani wake wanaweza kukwambia kuwa Raila Odinga ni mwanasiasa ambaye kwa miaka kadhas sasa amekuwa moto unaoendesha mashine ya siasa za Kenya. Katika miaka ya mwanzoni ya 90 alikuwa mbele kuongoza juhudi za upinzani, wakati wa utawala wa Rais Mwai Kibaki alikuwa waziri mkuu, lakini katika kipindi cha miaka 10 iliyopita amerejea kuwa kinara wa upinzani nchini Kenya.
Katika historia yake ndefu kwenye siasa za Kenya Raila Odinga amekuwa katika vyama mbali mbali vya siasa wakati huu wote akitafuta mkusanyiko bora, unaofaa, unaokubalika, unaoweza kumfikisha katika ndoto yake ya kuwa rais wa Kenya.
Mwaka huu, kwa mara nyingine tena, anadhani amepata ushirika ulio bora – ushirika wa NASA – National Super Alliance – ambao utamwingiza ikulu.
Ingawa amejijengea jina lake mwenyewe katika siasa za Kenya, Raila amesaidiwa pia na jina lake la mwisho Odinga. Baba yake, Jaramogi Oginga Odinga, alikuwa miongoni wa wapigania uhuru wa kwanza wa Kenya na aliwahi kuwa makamu rais baada ya uhuru.
Muda mfupi baada ya uhuru, Jaramogi Odinga aliiwacha nafasi ya makamu rais baada ya kutofautiana na rais wa wakati ule Jomo Kenyatta na kuanza kuongoza harakati za siasa za upinzani nchini Kenya.
Raila Odinga alifuata nyayo za kisiasa za baba yake na mwaka 1982 alishutumiwa kwa jaribio la kuipindua serikali ya rais Daniel arap Moi na kuwekwa kizuizini kwa miezi saba.
Hii itakuwa mara ya nne kwa Raila Odinga kugombea urais na katika majaribio yake yote hayo huenda huu ni mwaka ambapo ama apate la sivyo itakuwa mwisho mwa fursa yake kuwa rais wa Kenya. Raila odinga ana umri wa miaka 72.
Siasa za Raila Odinga zinaweza kuzungumziwa kama demokrasia ya kijamii yenye sera za kiliberali. Kuna wakati alikuwa anapendelea zaidi mfumo wa nguvu za bunge,ndio sababu aliunga mkono mabadaliko ya katiba kutaka nguvu za madaraka kwa waziri mkuu lakini baadaye alibadili pia mwelekeo na kuunga mkono mfumo wa urais ambao madaraka yake yanadhibitiwa kwa kiwango fulani na mfumo wa ugatuzi unaotumika sasa nchini Kenya.