Mratibu wa Mkoa wa Pwani John Elungata ametoa ripoti hiyo masaa kadhaa baada ya shambulio la kushitukiza katika eneo la Nyongoro, sehemu maarufu ambayo Al-Shabaab imekuwa ikifanya mashambulizi yanayo lenga abiria katika magari na vyombo vya usalama.
Watu watatu waliuawa na wengine watatu kujeruhiwa vibaya sana wakati washukiwa wa wapiganaji wa Al-Shabaab waliposhambulia basi lililokuwa linaelekea Lamu kutoka Mombasa.
Magaidi hao imefahamika kuwa walikuwa wanajaribu kulazimisha basi lisimame lakini dereva aliongeza mwendo, na hivyo ikawafanya walirushie basi hilo risasi.
Kamishna wa Kaunti Irungu Macharia amesema wale waliouawa na wengine waliojeruhiwa hawajaweza kutambuliwa hadi hivi sasa.
Timu za maafisa usalama zilipelekwa katika eneo la Nyongoro na maeneo yanayo lizunguka ili kukabiliana na wale waliowashambulia watu hao kwa bunduki.
Shughuli za usafiri zilisitishwa katika barabara ya Lamu-Garsen baada ya mabasi yaliyokuwa yanaelekea Mombasa kutoka Lamu na yale yanayo toka Lamu kwenda Mombasa yalilazimishwa kurudi Kituo cha Polisi cha Witu.