Katika mkutano na waandishi wa habari Jumatano jijini Dar es salaam, mkuu wa mkoa Paul Makonda ametaja orodha ya watu 65 wanaotakiwa kuripoti polisi Ijumaa wiki hii.
Washukiwa hao ni pamoja na mbunge mstaafu wa kinondoni (CCM), Iddi Azan, mfanyabiashara maarufu, Yusuph Manji, mchungaji Josephat Gwajima na watu wengine binafsi wakiwemo wafanyabiashara wanaomiliki mahoteli, kasino, meli na wamiliki wa vituo kadhaa vya mafuta.
Your browser doesn’t support HTML5
Hatua hii ni kile Makonda alichokiita ni awamu ya pili ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya katika mkoa wa Dar es Salaam.
Mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili ameripoti kuwa Chadema imelaani hatua hiyo ya kumhusisha mwenyekiti wao na biashara ya madawa ya kulevya.
Katibu mkuu wa Chadema, Dkt Vincent Mashinji alielezea kutoridhishwa kwao na utaratibu uliotumiwa na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam kutoa tuhuma dhidi ya mwenyekiti wao wa taifa
Katika hatua nyingine CHADEMA pia wamezungumzia kutoridhishwa na kukamatwa kwa mwanasheria wa chama hicho na mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ambaye mpaka sasa anashikiliwa na polisi
Katika mkutano na waandishi wa habari kituo kikuu cha polisi jijini Dar es Salaam kamanda wa polisi kanda maalum ya Dar es salaam Simon Sirro alithibitisha kukamatwa kwa Lissu.
Lissu alikamatwa Jumatatu wiki hii katika maeneo ya bunge mjini Dodoma alipokuwa akihudhuria vikao vya bunge vinavyoendelea na kurejeshwa jijini Dar es salaam na toka wakati huo anashikiliwa na polisi