Washukiwa 13 wa mauaji ya wanawake Uganda wafikishwa mahakamani

Washukiwa 13 wa mauaji ya wanawake katika mji wa Entebbe wamefikishwa mahakamani na kufunguliwa mashtaka ya ugaidi, wizi wa kimabavu na mauaji.

Hatua ya kufunguliwa mashtaka kwa washukiwa hao 13, inajiri siku moja baada ya spika wa bunge la Uganda Bi Rebecca kadaaga kuamrisha waziri wa usalama na waziri wa maswala ya ndani kuhakikisha kwamba wahusika wa mauaji hayo wanakamatwa na kushitakiwa.

Mbele ya jaji Jamson Karemani katika mahakama ya Nabweru nje ya jiji la Kampala, washukiwa wamefunguliwa mashtaka ya ugaidi, wizi wa kimabavu na mauaji.

Wanashutumiwa kuwaua wanawake 28 katika maeneo ya Entebbe na manispaa ya Nansana, Kao, na Kawempe, kati ya mwezi mei na agosti 2017.

Baadhi ya washukiwa hao ni Ibrahim Kaweesa, Robert Mugerwa, Tamale Isma,Steven Ssempijja, Mahad Kakumba, Sam Mayambala,Philip Tumuhimbise, Tina Prosper Nantongo, David Wasswa,George Ssempa, Bosco Waligo na Ismeal Ssegawa. Wana umri kati ya miaka 19 na 38.

Mauaji hayo ya wanawake kati ya umri wa miaka 20 na 35 kuuawa vimekuwa vikiripotiwa katika manispaa ya Entebbe na Nansa kwa mda sasa. Wanawake hao wamekuwa wakibakwa, kuuawa na vijiti kuingizwa katika sehemu zao za siri.

Sababu ya mauaji hayo haijafahamika, lakini polisi wanadai mauaji hayo ni ya kishirikina kwa imani za kupata utajiri.

Ilitarajiwa kwamba washukiwa 30 walio mikononi mwa polisi wangefikishwa mahakamani leo hii lakini taarifa imetolewa kwamba wengine bado wanafanyiwa uchunguzi.

Washukiwa hawakuruhusiwa kukataa au kukubali mashtaka, kwa sababu mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi inayowakabili. Wanazuiliwa katika gereza la Luzira hadi tarehe 21 mwezi septemba wakati kesi yao itakapoanza kusikilizwa huku uchunguzi zaidi ukiendelea.

Mashtaka yanayowakabili yana adhabu ya kifo kwa kunyongwa.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennes Bwire, Uganda.