Wakati NATO ikijiandaa kukutana Jumanne kwa mkutano wa siku tatu mjini Washington kwa maadhimisho ya miaka 75, muungano huo unaimarisha uungaji mkono wake kwa Ukraine katika vita vinavyoendelea na Russia.
Katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumapili akitathmini maandalizi ya mkutano huo, Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg alisema wanachama wote wa NATO wanataka amani, na hilo linaweza kupatikana kama Rais wa Russia Vladimir Putin anaelewa hawezi kushinda kwenye uwanja wa vita.
Njia ya haraka ya kumaliza vita hivi ni kushindwa vita, alisema. Lakini hilo halitaleta amani. Hili litaleta ukaliaji kimabavu. Stoltenberg alielezea hatua muhimu ambazo NATO itachukua, ikijumuisha kuanzishwa kwa amri kamandi ya kijeshi nchini Ujerumani, kuimarisha misaada ya kifedha na kijeshi, na mikataba ya ulinzi ya pande mbili.