Juhudi za karibuni za chama cha Republican kuufanyia mageuzi mfumo wa taifa wa huduma nafuu za afya zinaonekana kushindikana baada ya seneta mwingine mrepublican kujitokeza dhidi ya mpango huo.
Seneta Susan Collins wa jimbo la Maine amekuwa ni seneta watatu mrepublican kupinga hatua hiyo aliposema Jumatatu usiku “hii si njia ya kutumia ambayo tunatakiwa tuifuate kushughulikia suala muhimu na lenye mkanganyiko ni lazima lishughulikiwe kwa umakini mkubwa na iwe haki kwa wamarekani wote”.
Tangazo la Collins limekuja baada ya ofisi ya bajeti bungeni kusema jaribio la kufuta sheria ya huduma nafuu za afya inayojulikana kama Obamacare itapunguza bima kwa mamilioni ya watu. Ikiwa na viti 52 katika baraza la senate lenye wanachama 100 warepublican hawawezi kumudu kupata kura mbili za hapana kutoka kwenye chama chao kama wanataka mswaada wa mageuzi ya afya upitishwe hasa ukiangalia kuwa upinzani wa Democrat uko pamoja.
Awali seneta John McCain wa jimbo la Arizona na Seneta Rand Paul wa jimbo la Kentucky tayari wametangaza upinzani wao kwa mpango huo.