Waraka wa Nunes wazua utata Marekani

Devin Nunes

Kamati ya Usalama ya Bunge imetoa waraka ambao unautata mkubwa ukionyesha madai yaliotolewa na Warepublikan kwamba maafisa wa ngazi ya juu wa usalama walitumia vibaya madaraka waliopewa kuchunguza kuingilia kati kwa Russia wakati wa uchaguzi wa urais 2016 nchini Marekani.

Waraka huo ulitolewa kwa umma Ijumaa, muda mfupi baada ya Rais Donald Trump kupitisha kuwa waraka huo sio siri tena, ambao uliandikwa na Mwenyekiti wa Kamati, Mbunge wa Republikan Devin Nunes.

Sehemu kubwa ya waraka huo umejikita katika sheria inayotoa idhini ya ufuatiliaji wa ujasusi wa nje ya nchi (FISA) ambao uliruhusu FBI kumchunguza aliyekuwa mshauri wa sera za kigeni katika Kampeni ya Trump, Carter Page, ambaye ni mfanyabiashara mwenye maslahi nchini Russia. Kulikuwa na ukakasi juu ya madai ya kuwa Pages alikutana na wawakilishi wa idara ya ujasusi ya Russia.

Waraka huo unasisitiza kuwa taarifa iliyokuwa imetayarishwa na aliyekuwa jasusi wa Uingereza Christopher Steele ilikuwa ni “sehemu muhimu” ya matumizi ya Sheria ya FISA katika kumchunguza Page, na kuwa Shirika la Upelelezi la FBI haikuweka wazi kuwa taarifa ya Steele ilikuwa imedhaminiwa na kampeni ya Hillary Clinton na kamati ya taifa ya chama cha Demokrat, au Steele siku za nyuma aliwahi kutoa matamko dhidi ya Trump.

Msimamo wa Trump

Akizungumza na waandishi ikulu ya White House Ijumaa, Trump ameeleza kuwa maudhui ya waraka huo ni yakusikitisha. Nafikiri ni aibu kubwa kile kinachoendelea katika nchi hii… Watu wengi lazima waone aibu na zaidi ya hapo.

Alipoulizwa na mwandishi iwapo kutolewa kwa waraka huu kunaashiria kuwa upo uwezekano mkubwa wa Naibu Mwanasheria Mkuu Rod Rosenstein kufukuzwa kazi, Trump amejibu, “ tafuta hilo mwenyewe.”

Rosenstein anasimamia uchunguzi dhidi ya Russia na ndiye aliyemchagua mwendesha mashtaka maalum Robert Mueller kuongoza uchunguzi huo.

Mvutano uliopo Marekani

Kutolewa kwa waraka huo kunaongeza mvutano kati ya Trump na wafuasi wake ndani ya chama cha Republikan kwa upande moja, na Wademokrat na uongozi wa juu wa FBI upande mwengine iwapo uchunguzi juu ya Russia kuingilia kati uchaguzi wa urais uliathiriwa na upendeleo wa kisiasa kwa upande wa wachunguzi.

Nunes ametoa tamko Ijumaa likieleza matumaini yake kuwa hatua zilizochukuliwa na Warepublikan katika kamati ya usalama zitapelekea “kutoa mwanga” kwa kile alichokiita “ni mtiririko wa matukio ya kuogopesha.”

“Kamati hiyo imegundua ukeukaji mkubwa wa dhamana ya umma, na watu wa Marekani wanahaki kujua pale maafisa katika taasisi muhimu wanapotumia madaraka yao vibaya kwa sababu za kisiasa,” Nunes amesema.

“Taasisi zetu za usalama na ulinzi zipo kwa ajili ya kuwalinda wananchi wa Marekani, sio kwa ajili ya kutumika kuwalenga kikundi kimoja kwa ajili ya maslahi ya kikundi kingine.

Msimamo wa Spika

Kwa upande wake Spika wa Bunge la Marekani Paul Ryan ametoa tamko Ijumaa akisema “wasiwasi ulioelezwa” katika waraka huo ni “wakweli.” Amesema anaunga mkono kutolewa kwa waraka wa Nunes na pia waraka wa Wademokrat waliowachache katika bunge.

Ni muhimu tuangalie kwa makini zaidi hatua mahsusi na watendaji mahsusi na tusitumie waraka huu kutilia mashaka uadilifu wa mifumo ya sheria na FBI, ambayo inaendelea kuwatumikia wananchi wa Marekani kwa uadilifu,” Ryan amesema.

Hisia za Wademokrat

Wajumbe wa chama cha Demokrat walio wachache katika kamati wametoa tamko refu wakishambulia uamuzi wa Nunes kutoa waraka huo. Tamko hilo limesema kuwa waraka huo unamadai yanayopotosha yale yaliojiri katika Idara ya sheria na Shirika la Upelelezi (FBI) na kuwa ni juhudi za kutia dosari na kujaribu kuchafua taasisi, na kurudisha nyuma uchunguzi unaoendelea kufanywa na mwendesha mashtaka maalum, na kudhoofisha uchunguzi unaofanywa na Bunge la Congress.

Tamko la Wademokrat limewatuhumu Warepublikan kwa kuweka “msingi mbaya” kwa kutoa waraka huo wa siri ambao utakuwa na athari mbaya ya muda mrefu kwa jamii ya wana usalama, kwa minajili ya kumhami Trump dhidi ya tuhuma zitakazo pengine mkabili katika uchunguzi unaofanywa dhidi ya Russia.

Tamko la Mwanasheria Mkuu

Kwa upande wake Mwanasheria Mkuu Jeff Sessions ametoa tamko juu ya waraka huo Ijumaa, akisema, "yeye ana imani kubwa na wanaume na wanawake wa idara hii ya sheria. Lakini hakuna idara ambayo haina dosari.

Kama kawaida, nitapeleka habari yote hii juu ya suala hili nilioipokea kutoka bunge la congress kwa wahusika katika idara ya sheria."

Rais wa Umoja wa wakala FBI Thomas O’Connor ametoa tamko Ijumaa akiwatetea maafisa wa ngazi zote za shirika la FBI na utayari wao wa kutumikia katika nafasi zao.

“Watu wa Marekani ni lazima wafahamu kuwa wanaendelea kutumikiwa kwa moyo wa dhati na Shirika la Dunia lililo maarufu lenye kusimamia sheria,” tamko hilo limesema.

“Wafanyakazi maalum wa FBI hawajawahi na wala hawatofanya hilo, la kuelemea upande moja wa kisiasa ili kutuzuia sisi kutekeleza majukumu tulioahidi.