Takriban watu 19 wamepatikana wakiwa wamekufa na wengine wawili hawajulikani walipo baada ya maporomoko ya ardhi katikati mwa Indonesia, viongozi wa eneo hilo wamesema Jumapili.
Waliofariki na manusura wawili walihamishwa kutoka vijiji viwili vilivyokumbwa na maporomoko ya udongo katika eneo la Tana Toraja, jimbo la Sulawesi Kusini Jumamosi jioni, amesema mkuu wa shirika la maafa Sulaiman Malia.
“Kumekuwa na vifo 19, na vinne huko Makale Kusini na wengine 15 katika vijiji vya Makale,” Malia ameiambia AFP Jumapili.
Aliongeza kusema kwa muda huo walikuwa wanaendelea kuwatafuta wengine walio athirika, akiongeza kuwa bado kuna watu wawili walioripotiwa kupotea ambao huenda wamefukiwa na vifusi vya maporomoko ya ardhi.
Tana Toraja na maeneo yanayoizunguka yamekumbwa na mvua nyingi mara kwa mara, hasa katika kipindi cha wiki moja iliyopita, bila kusimama, Malia aliongeza kusema.