Wawili kati ya wagombea wakuu wa upinzani kwenye uchaguzi wa Disemba mwaka jana nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wameitisha maandamano Jumamosi, wakati wa kuapishwa kwa Rais Felix Tshisekedi kuongoza muhala wa pili.
Tshisekedi alishinda kwa kishindo uchaguzi wa tarehe 20 Disemba, lakini uchaguzi huo uligubikwa na madai mengi ya udanganyifu, changamoto za kiufundi na kasoro nyingine.
Viongozi wawili wa upinzani, Martin Fayulu na Moise Katumbi pamoja na wapinzani wengine, waliomba uchaguzi mpya, ombi ambalo lilitupiliwa mbali na serikali.
“Tuna maandamano Januari 20 kwa sababu hatukukubali matokeo, kulikuwa udanganyifu kila mahali na lazima uchaguzi ubatilishwe,” amesema Katumbi katika mkutano na waandishi wa habari kwa njia ya mtandao.