Vyanzo vya habari nchini Burundi vimesema kuwa kampeni hizo zimekumbwa na mvutano, wakiwemo wale wanaoona kuwa ni mbinu ya kubadilisha katiba kwa maslahi ya Rais Pierre Nkurunzinza.
Wanasema kuwa kuna uwezekano mkubwa zikampa nafasi Rais huyo kuendelea kutawala kwa miaka 14 huko siku za usoni.
Nkurunzinza ameongoza nchi hiyo kwa kipindi cha miaka 13 hadi sasa na wapinzani wake wamekuwa wakimtaka aachie madaraka kwa sababu ni kinyume cha sheria kugombea nafasi ya urais kwa mara nyingine.
Wachambuzi wa kisiasa wanasema kuwa kura ya maoni hiyo ina dhamiria kuanzisha mchakato wa kubadilisha katiba kwani serikali ya Nkurunzinza inadai kuwa katiba iliyoko haiendi na wakati.
Pia kwa mujibu wa wapinzani serikali ina nia yakuondoa kipengele cha ukomo wa mihula miwili anayohudumu rais - miaka mitano kila mmoja.
Mabadiliko yanayopendekezwa ni pamoja na kuwepo wadhifa wa waziri mkuu na kupunguza idadi ya makamu wa rais wawili kuwa mmoja.
Kwa upande wao vyama vya upinzani vinadai kuwa mabadiliko hayo ya katiba yanatishia mkataba wa amani uliofikwa Agosti 28, 2000, Arusha uliosimamiwa na hayati Nelson Mandela akiwa ni mpatanishi. Pia viongozi wa dunia akiwemo Bill Clinton wa Marekani na marais wa kikanda akiwemo Rais mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa na Rais Yoweri Museveni wa Uganda walihudhuria katika makubaliano hayo.
Mkataba huo ulisaidia kumaliza vita vya kiraia nchini humo kati ya mwaka 1993 - 2006 yaliosababisha vifo vya zaidi ya watu laki tatu.