Wapalestina na Waisraeli wajeruhiwa katika ghasia ndani na nje ya Al-Aqsa

Wapalestina wakikusanyika katika uwanja wa Msikiti wa Al-Aqsa kufuatia mapambano na majeshi ya Israeli huko mji wa Old City, Jerusalem.

Zaidi ya Wapalestina na Waisraeli 20 wamejeruhiwa Jumapili kutokana na matukio mbali mbali ndani na karibu na uwanja wa msikiti wa Al-Aqsa, siku mbili baada ya kutokea ghasia kubwa katika eneo hilo.

Kutokana na mapambano ya leo idadi ya watu waliojeruhiwa tangu Ijumaa imefikia 170, wakati huu muhimu wa sikukuu ya Wayahudi ya Passover na mwezi wa Ramadhan kwa Waislamu.

Polisi wa Israel wanasema mapema hii leo mamia ya waandamanaji wa Kipalestina walianza kukusanyika ndani ya uwanja wa msikiti huo mtakatifu kwa waislamu na wayahudi, walikusanya mawe, muda mfupi kabla ya kuwasili wageni wa kiyahudi.

Polisi wanasema maafisa wake waliingia kwenye uwanja huo ili kuwaondoa waandamanaji na kurudisha utulivu.

Nje ya uwanja huo katika mtaa wa kale wa Jerusalem Mashariki inayokaliwa na Israel vijana wa Kipalestina wamekuwa wakirusha mawe kwenye mabasi yaliyokuwa yanapita na maafisa wa hospitali walisema watu 7 walijeruhiwa.

Polisi inasema imewakamata wapalestina 18.

Mfalme Abdullah wa pili wa Jordan ambaye taifa lake la Kifalme lina mamalaka ya maeneo takatifu ya Jerusalem Mashariki yaliyotekwa na Israel wakati wa vita vya 1967 na baadae kukaliwa na Israel, ametoa wito Jumapili kwa Israel kusitisha mara moja hatua zozote zisizo ambatana na sheria na za uchokozi zinazozidisha ugomvi.