Wapalestina 13 waliuawa katika shambulizi lililofanywa na Israel

Moshi uliotanda kutokana na mlipuko wakati wa operesheni ya kijeshi ya israel kwenye kambi ya wakimbizi ya Nur Shams. April 20, 2024.

Israel imesema wanajeshi wake waliwaua magaidi 10 na kuwakamata wanane katika kambi ya wakimbizi ya Nur Shams

Wapalestina wasiopungua 13 waliuawa katika shambulio lililofanywa na vikosi vya Israel katika eneo linalokaliwa kimabavu la Ukingo wa Magharibi, vikosi vya Israel na Palestina vimesema Jumamosi.

Israel imesema wanajeshi wake waliwaua magaidi 10 na kuwakamata wanane wakati wa shambulizi katika kambi ya wakimbizi ya Nur Shams, ambalo lilianza mapema Ijumaa. Kundi la wanamgambo la Islamic Jihad limesema wanachama wake watatu waliuawa.

Kundi la Tulkarm Brigades, ambalo linajumuisha vikosi kutoka makundi tofauti ya Wa-palestina, limesema wapiganaji wake walipambana kwa silaha na vikosi vya Israel siku ya Jumamosi. Waandishi wa shirika la habari la AFP walisikia milio ya risasi, waliona miili ikiwa imelala barabarani na nyumba zilizoharibiwa na ndege zisizo na rubani za Israel.

Jeshi la Israel limesema mapigano hayo yalidumu kwa zaidi ya saa 40 na kwamba wanajeshi wake wanane na afisa mmoja wa polisi walijeruhiwa.