Wanawake waomba nafasi zaidi za uongozi Tanzania

  • VOA News

Baadhi ya wanawake wa Tanzania waliokutana katika siku ya Kimataifa ya Wanawake.

Wakati dunia ikiadhimisha siku ya Kimataifa ya Wanawake Ijumaa Machi 8, nchini Tanzania wanawake wametakiwa kuongeza juhudi zao katika siasa, ili kuhakikisha kuna wingi wa viongozi wanawake nchini.

Mkurugenzi wa kituo cha sheria na haki za binadamu (LHRC), Anna Henga, alisema kuwa kuwapatia wanawake fursa katika uongozi kuanzia ngazi za chini kutasaidia kuwasilisha ajenda zao, na taasisi yake imejipanga kuhakikisha wanapatikana viongozi wanawake katika serikali za mitaa.

Kwa mujibu wa kituo cha sheria na haki za binadamu Tanzania ina asilimia 2.1% ya wanawake wenyeviti wa vijiji, asilimia 6.7% ya wenyeviti wa vitongoji pamoja na asilimia 12% ya wenyeviti wa mitaa, hiyo ikiwa idadi ndogo ikilinganishwa na idadi ya vijiji na vitongoji vilivyopo nchini.

Wakili Fatma Karume, aliyewahi kuwa rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, (TLS) anasema kuna haja ya kuzitathmini upya sheria za uchaguzi kwa kuwa zimekuwa zikitoa nafasi chache kwa wanawake kuingia katika vyombo vya maamuzi suala linalowakwamisha juhudi za wanawake kuingia kwenye nafasi za uongozi.

Kauli mbiu ya mwaka huu ilikuwa ni wekeza kwa wanawake kuharakisha maendeleo ya taifa na ustawi wa jamii.