Wanawake Somalia wanataka kutengewa 30% ya viti vya bunge

Wabunge wa Somalia katika mojawapo ya vikao vya bunge

Wanawake wanashikilia asilimia 24 ya viti 329 katika bunge la Somalia.

Makundi ya kutetea haki za wanawake, wafanyabiashara mashuhuri na wanasiasa wanawake nchini Somalia wanataka bunge la nchi hiyo ambalo idadi kubwa ya wabunge ni wanaume, kupitisha mswada utakaohakikisha kwamba asilimia 30 ya viti vya bunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao, vinatengewa wanawake.

Wanawake wanashikilia asilimia 24 ya viti 329 katika bunge la Somalia.

Bunge la chini la Somalia, lilipitisha mswada mwezi Juni, unaoruhusu asilimia 30 ya viti vya bunge kutengewa wanawake, lakini mswada huo haujafikishwa mbele ya bunge la juu kwa mdala na kupigiwa kura.

Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Mohamed alisaini makubaliano na viongozi wa kanda mnamo mwezi Septemba, uliojumulisha asilimia 30 ya viti vya bunge, lakini makundi ya kutetea haki za wanawake yanasema kwamba makubaliano hayo pekee hayatoshi.

“Tunataka makubalino haya ya kutenga asilimia 30 ya viti vya bunge kwa wanawake kuwa sheria,” amesema Deqa Abdiqasim Salad, mkurugenzi wa shirika la wanawake kwa jina ‘Hear Women’, yaani, msikilize mwanamke.

Shirika hilo linashughulikia harakati za wanawake katika siasa.

“Tunafuraha kwamba tumepata asilimia 24 ya viti tulivyo navyo bungeni kwa sasa lakini kuwepo sheria ni muhimu sana ili kuhakikisha kwamba hatupotezi vipi tulivyo navyo na tupate nguvu za kuimarisha demokrasia kwa kuwa na waakilishi wengi katika kufanya maamuzi ya sera.” Ameendelea kusema Salad.

Salad ni mmoja wa wanaharakati zaidi ya 135 wanaotaka sheria ya kutenga asilimia 30 ya viti vya bunge kwa wanawake.

Wengine ni Pamoja na mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi ya kitaifa Halima Ismail Ibrahim, Daktari maarufu Amina Aden Mohamed na mwanaharakati wa haki za wanawake Luul Maxamed Feerayare. Wabunge 79 wanawake katika bunge la sasa la Somalia, ni miongoni mwa watu wanaosukuma mswada huo upitishwe.

Wanaounga mkono mswada huo wanataja mafanikio yaliyopatikana katika naadhi ya nchi za Afrika kama Rwanda, inayoongoza ulimwengu kwa kuwa na asilimia 55 ya viti vya bunge kwa wanwake.

Katiba ya Rwanda inatenga asilimia 30 ya nafasi katika kamati zote zinazofanya maamuzi ya sera za serikali, kwa wanawake.

Wanawake nchini Somalia wamechangia sana katika kurejesha nchi hiyo katika hali ya utulivu na maendeleo tangu kutokea vita mwaka 1991, na sasa wanasema wana haki ya kuwa na mchango dhabithi bungeni.

Uchaguzi wa Somalia unatarajiwa kufanyika Februari 2021.

Nchi hiyo ya Afrika mashariki ina viwango vya juu vya Watoto wasichana kuoleka, manyanyaso dhidi ya wanawake, kunajisiwa na ukeketaji wa wanawake.

Umoja wa mataifa unasema kwamba asilimia 45 ya wanawake nchini Somalia huoleka kabla ya kutimia umri wa miaka 18 na asilimia 98 hukeketwa.

Makundi ya kutetea haki za wanawake yanasema kwamba yanahitaji kuakilishwa vipasavyo katika utungaji sheria ili kukomesha maovu dhidi ya wanawake nchini humo.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC