Wanasiasa wa upinzani waendelea kukamatwa Tanzania

John Magufuli - Rais wa Tanzania

Mwanasiasa wa upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu, alikamatwa kwa muda na kuachiliwa Jumatatu baada ya polisi kusema wamefanikiwa kuzima maandamano yaliyokuwa yameitishwa na waupinzani kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa wiki iliyopita.

Wanasiasa kadhaa wa upinzani wamekamatwa wakati na baada ya matokeo ya uchaguzi huo kutangazwa.

Wanasiasa hao wanataka uchaguzi mkuu wa Tanzania kurudiwa wakisema ulikuwa na dosari chungu nzima.

Wameitisha maandamano ya amani nchi nzima kupinga ushindi wa asilimia 84 wa rais John Magufuli.

Chama kikuu cha upinzani Chadema, hakijatoa ripoti zaidi kuhusu kukamatwa kwa Lisu, vile vile maafisa wa polisi hawajaeleza sababu zilizopelekea kukamatwa.

Kupitia ukurasa wa Twitter, Chadema kimesema kwamba kiongozi wao ameachiliwa huru baadaye. “Hatujafanikiwa kuandamana,” Lissu ameambia shirika la habari la Reuters.

Maafisa wa polisi wameshika doria katika miji kadhaa ya Tanzania kuzima maandamanao hayo huku wanasiasa wa upinzani kadhaa waliokuwa wametangaza kuongoza maandamano hayo wakiwa wamekamatwa na polisi na kuzuiliwa.

Miongoni mwa waliokamatwa na polisi ni Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, aliyekuwa mbunge wa Arusha Godbless Lema na aliyekuwa meya wa manispaa ya Ubungo Boniface Jacob.

Kulingana na Kamanda wa polisi wa Dar-es-salaam Lazaro Mambosasa, Mbowe, Lema, Jacob, na watu wnegine saba ambao ni wafuasi wa chama hicho, wamekamatwa katika hatua ya kuzuia uharibifu wa mali kwa kisingizio cha kufanya maandamano.

“Tunatafuta wengine. Tangu tumeanza kuwakamata washukiwa, wanasiasa wa upinzani wamejizuia na mji ni mtulivu,” amesema Mambosasa.

Kulingana na sheria za Tanzania, mshukiwa anaweza kukamatwa na kuzuiwa kwa saa 24 bila kufunguliwa mashtaka mahakamani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo ameandikwa ujumbe wa twiter kwamba Marekani itachunguza ripoti za maafisa wa usalama Tanzania kutumia nguvu dhidi ya raia wakati wa uchaguzi huo.

“Tumesikitishwa sana na ripoti za kutokea udanganyifu katika uchaguzi wa Tanzania, wanasiasa wa upinzani kukamatwa kwa sababu za kisiasa na kutokea ghasia nchini humo wakati wa uchaguzi wa wiki iliyopita. Tunahimiza mamlaka kushughulikia mambo hayo,” ameandika Pompeo.

Wiki iliyopita, Tanzania iliripoti ukosefu wa huduma ya internet na mitandao ya kijamii kote nchini, ikiwemo Twitter na Whatsapp.

Wakosoaji wametaja hatua hiyo kama juhudi za kuzuia mawasiliano.

Chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo ambacho kimeungana na Chadema katika kupinga matokeo ya uchaguzi huo na kuhimiza wafuasi wao kuandamana, kimeta uchunguzi wa kimataifa kufanyika kuhusu uchaguzi huo na uchaguzi mpya kuandaliwa.

Tume ya uchaguzi imesema kwamba uchaguzi huo ulikuwa huru na haki na hakuna ushahidi wowote wa kufanyika udanganyifu kama kuwepo karatasi bandia ya kupigia kura.

Chama cha Magufuli CCM, ambacho kimetawala Tanzania tangu kupata uhuru mwaka 1961, kimepata asilimia 97 ya viti vya bunge.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC