Wanasiasa watatu wa upinzani wa Uganda wamewekwa rumande usiku wa kuamkia maandamano yaliyopigwa marufuku dhidi ya ufisadi, polisi wamesema Jumatatu, huku kiongozi wa upinzani Bobi Wine akisema kuwa vikosi vya usalama vilivyojihami vilikuwa vinazingira makao makuu ya chama chake.
Hatua hiyo inajiri siku mbili baada ya Rais Yoweri Museveni, ambaye ametawala nchi hiyo kwa ukali kwa takriban miongo minne, kuonya kwamba Waganda wanaopanga kuingia mitaani Jumanne wanacheza na moto.
Wabunge watatu na watu wengine saba wamefikishwa mahakamani leo, wakishtakiwa kwa makosa mbalimbali na kurudishwa gerezani, msemaji wa polisi wa Uganda Kituuma Rusoke ameiambia AFP mwishoni mwa Jumatatu, bila kutoa maelezo zaidi kuhusu mashtaka yanayowakabili wanasiasa na watu hao.