Wananchi wa Jordan wanaendelea na maandamano dhidi ya sheria ya mapato iliyopangwa kuanzishwa, wakiahidi kuwa wataendelea kushinikiza serikali ifanye mabadiliko.
Maandamano ya siku ya Jumatano huko Amman yametokea wakati walioandaa maandamano hayo wakiitisha tena mgomo wa siku moja.
Siku za karibuni, waandamanaji na maafisa wa usalama walipambana katika mitaa mbalimbali nchini humo.
Waadamanaji wanashinikiza serikali kuacha kuongeza bei ya bidhaa na mpango wa kuongeza kodi ambapo wakosoaji wa sera hizo wanasema zinawalenga maskini na watu wa kipato cha kati.
Mfalme Abdullah amechukua hatua kujibu matakwa ya waandamanaji kwa kumteua waziri mkuu mpya Jumanne.
Viongozi wa kimataifa wameshinikiza kuwepo mageuzi ya kiuchumi kusaidia kupunguza deni la taifa la Jordan, linalotokana na uchumi kulegalega kwa sababu ya machafuko katika eneo hilo.