Wanamgambo wa Al Shabab wauwawa Jubaland

Wanamgambo wa kundi la kigaidi la Somalia la Al-Shabaab

Dazeni za wanamgambo wa al-Shabab wameuwawa katika mapigano mapya katika jimbo la Jubaland kusini, maafisa wamesema.

Mapigano hayo yalifuatia mashambulizi matatu tofauti yaliyoratibiwa ya wanamgambo hao katika kambi za kijeshi zinazosimamiwa na vikosi vya serikali na kikanda magharibi na kusini mwa mji wa Kismayo.

Wanamgambo hao wameshambulia Bulo Haji, Harbole, na Mido, miji ambayo yote ilitwaliwa kutoka kwa al-Shabab toka mwezi uliopita.

Wanamgambo hao pia walifyatua risasi kwenye kambi ya nne ya Bar Sanuni katika jaribio la kuleta tafrani baada ya kuimarishwa ulinzi wa kambi hizo zinazoshambuliwa.

Msemaji wa jeshi la eneo la Jubaland, Meja Mohamed Farah Dahir, ameiambia VOA kwamba wanamgambo 135 waliuawa katika mashambulizi hayo.