Wanajeshi wazingira Tigray, masaa 72 ya kujisalimisha yamemalizika

Raia wa Ethiopia wanaokimbia mapigano Tigray wakijitayarisha kuvuka mto Setit kuingia Sudan Nov. 14, 2020.

Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, amekataa kile alichosema kama jamii ya kimataifa kuingilia kati mgogoro wa Tigray ambapo muda wa saa 72 aliotoa kwa vikosi vya Tigray kujisalimisha ulimalizika Jumanne usiku.

Mamia ya watu wameripotiwa kuuawa tangu vita hivyo vilipoanza Novemba 4, na zaidi ya watu 41,000 wamekimbilia Sudan kama wakimbizi.

Mtafiti wa shirika la Amnesty international anayefuatilia mapigano hayo amesema kwamba vikosi vya Tigray ndiyo vimehusika na mauaji ya mamia ya watu kutoka kabila la Amhara, katika mji wa Mai-Kadra.

Watafiti wanaofanya kazi na shirika lisilo la kiserikali wamekuwa wakitumia picha na video pamoja na kufanya mahojiano na watu walioshuhudia matukio mbali mbali kujua yanayoendelea katika mapigano ya Tigray.

Makaburi yaongezeka, maiti kando mwa barabarani

Kuna makaburi ambayo watu wamezikwa katika siku za karibuni, katika sehemu yalipo makanisa, mjini Mai-Kadra.

Maiti wametapakaa kando mwa barabara na kuanza kuoza, magharibi mwa Tigray.

Mtafiti wa shirika la Amnesty international nchini Ethiopia na Eritrea Fisseha Tekle, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba wanajeshi wa Tigray walishindwa katika vita vilivyotokea adhuhuri Novemba 9 nje ya mji wa Mai Kadra, na kuondoka sehemu hiyo hadi katika mji wa Mai Kadra.

Amesema kwamba mauaji makubwa yalitokea mjini humo na mamia ya watu wamepoteza maisha.

"Tumezungumza na waathirika, wengine wao wamekimbilia Gondar, na waliojeruhiwa wanapatiwa matibabu katika hospitali ya Gondar. Wametuambia kwamba wapiganaji wa utawala huo na makundi ya vijana kutoka jamii ya Tigray walikuwa wanawalenga watu wa Amhara." Amesema Fisseha Tekle.

Haya ndio mapigano mabaya zaidi kuwahi kutokea dhidi ya raia katika vita vinavyoendelea kaskazini mwa Ethiopia.

Utawala wa Abiy wafutilia mbali madai

Serikali ya waziri mkuu Abiy Ahmed imefutilia mbali madai hayo na kuendelea kushambulia utawala wa eneo la Tigray.

Wakimbizi wa Tigray waliokimbilia Sudan kutoka Mai-Kadra, wanasema kwamba vikosi vya serikali ndivyo vilivyotekeleza mauaji hayo wakati waliposhambulia mji huo wenye wakaazi 40,000.

Kiongozi mpya wa Mai Kadra, Fentahun Bihohegn amesema kwamba "Mashambulizi hayo ni ya kikabila. Mauaji mabaya ya kikabila yamefanyika dhidi ya watu wa Amhara. Nimeshuhudiza jehanamu hapa Mai-Kadra.”

Vikosi vya serikali vyazingira Tigray

Magari ya kijeshi na silaha nzito vinaripotiwa kuzingira mji mkuu wa Tigray ambapo Abiy ametishia kutekeleza mashambulizi mabaya ya mwisho iwapo wapiganaji wa eneo hilo hawatajisalimisha.

Waliokuwa marais watatu wa nchi za Afrika wamefika Addis Ababa, kujaribu kufanya mazungumzo kumaliza vita hivyo.

Kiongozi wa sera ya mambo ya nje wa umoja wa ulaya ameonya kwamba mapigano ya Ethiopia yanayumbisha eneo zima la Afrika mashariki.

Jamii ya kimataifa imekuwa ikisistiza kufanyika mazungumzo na kumaliza vita hivyo.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC