“Kwenye kambi ya MONUSCO huko Butembo, washambuliaji walipora silaha za polisi wa Congo na kuwafyatulia risasi wafanyakazi wetu waliovalia sare,” msemaji wa Umoja wa mataifa Farhan Haq amewambia waandishi wa habari kwenye makao makuu ya Umoja wa mataifa mjini New York.
Waandamanaji katika mji wa Butembo katika mkoa wa mashariki wa Kivu Kaskazini, wanaushtumu Umoja wa mataifa kushindwa kuwalinda dhidi ya ongezeko la mauaji yanayotekelezwa na makundi yenye silaha.
“Wanajeshi wetu wako katika tahadhari kubwa na wameshauriwa kujizuia kutumia nguvu, wakitumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji na kufyatua tu risasi za onyo hewani wakati wafanyakazi wa Umoja wa mataifa au mali zinaposhambuliwa,” Haq amesema.
Amesema mwanajeshi mmoja mlinda amani na maafisa wawili wa polisi waliuawa, huku mwingine akijeruhiwa.
Waziri wa mambo ya nje wa India ameandika kwenye Twitter kwamba walinda amani wawili wa India ni miongoni mwa waliouawa.
Mlinda amani kutoka Morocco pia ni miongoni mwa waliouawa, kulingana na vyombo kadhaa vya habari.