Wanajeshi watatu wa Marekani wauawa katika shambulio nchini Jordan

Ramani inayoonyesha kambi ya jeshi la Marekani nchini Jordan ambapo wanajeshi wa Marekani waliuawa katika shambulio la ndege isiyokuwa na rubani Jumapili

Wanajeshi watatu wa Marekani waliuawa na wengine 34 kujeruhiwa katika shambulio la ndege isiyokuwa na rubani lililotekelezwa na wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran kwenye kambi ya wanajeshi hao nchini Jordan, amesema Rais wa Marekani Joe Biden.

Ni shambulio la kwanza baya dhidi ya wanajeshi wa Marekani tangu vita kati ya Israel na Hamas kuzuka.

Shambulio hilo ambalo Iran inakanusha haikuhusika linaashiria hali ya mvutano mkubwa katika eneo la Mashariki ya kati, kukiwa na wasiwasi kwamba vita vya Israel dhidi ya Hamas vinaweza kuchochea mzozo mkubwa unaohusisha makundi yanayoungwa mkono na Iran huko Lebanon, Yemen na Iraq.

“Wakati bado tunakusanya taarifa kuhusu shambulio hilo, tunajua lilitekelezwa na makundi yenye itikadi kali yanayoungwa mkono na Iran yenye ngome huko Syria na Iraq,” Biden alisema katika taarifa.

Aliongeza kuwa “Bila shaka tutawawajibisha wale wote waliohusika kwa wakati na kwa namna tutaamua kufanya hivyo.”

Wanajeshi 34 wa Marekani walijeruhiwa katika shambulio la Jumapili kaskazini mashariki mwa Jordan karibu na mpaka wa Syria, kulingana na taarifa kutoka Kamandi ya Marekani.

Ujumbe wa Iran kwenye Umoja wa mataifa umesema katika taarifa leo Jumatatu kwamba Teheran haikuhusika katika shambulio hilo.