Tangazo hilo limekuja wakati ikulu ya Marekani pamoja na Pentagon wakiahidi kuendelea kuokoa wamarekani pamoja na watu wa Afghanistan walio hatarini nchini humo, ukisemekana kuwa uokozi mkubwa zaidi uliowahi kufanywa katika historia ya Marekani.
Wakati huo huo baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, Jumatatu limesema kwamba linatumai kwamba Taliban watahakikisha usalama wa watu wanaotaka kuondoka nchini humo.
Kati ya wanachama 15 wa baraza hilo, Russia na China hawakushiriki kwenye rasimu ya azimio hilo lililoandikwa na Marekani, Uingereza na Ufaransa na kuungwa mkono na mataifa mengine wanachama.
Baraza hilo liliangazia taarifa ya Taliban ya Agosti 27 kwamba hawatazuia watu wa Afganistan wanaotaka kuondoka nchini, iwe ni kwa barabara au ndege.