Wanajeshi wa Chad wameuawa katika mapigano na wanajihadi

Ramani ya Chad na nchi zilizo karibu nazo.

Rais wa Chad Mahamat Idriss Deby Itno alitoa salamu za rambirambi kwa familia na wale waliojeruhiwa kupitia Facebook.

Wanajeshi kadhaa wa Chad wameuawa katika mapigano na wapiganaji wa kijihadi katika mkoa wa Ziwa Chad, tukio la hivi karibuni katika taifa hilo la Afrika ya kati, maafisa wamesema Jumapili.

"Ninatoa rambirambi zangu za dhati kwa familia za wanajeshi waliofariki wakiwa wanailinda nchi wakati wa mapambano haya, na ninawaombea majeruhi wapone kwa haraka", Rais Mahamat Idriss Deby Itno alisema katika ujumbe kwenye mtandao wa Facebook, bila kutoa maelezo zaidi.

Mapigano hayo yalikuwa ya hivi karibuni tangu mwishoni mwa mwezi Oktoba, wakati wa shambulio lililofanywa na wanajihadi wa Boko Haram katika kambi ya jeshi ya Chad lililoua watu wasiopungua 40. Katika kujibu hilo, jeshi lilianzisha operesheni dhidi ya wanamgambo.

Katika taarifa yake, mkuu wa majeshi alisema Jumamosi kwamba kulikuwa na mapigano wakati wa mchana na baada ya saa kadhaa makundi mengi ya kigaidi yalidhibitiwa na kwamba idadi itatolewa baadaye.