Wanajeshi hao wametumwa kama sehemu ya kikosi cha kikanda kilichoundwa na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kujaribu kukomesha uasi wa kundi la M23 na kusambaratisha makundi takriban mia moja yenye silaha ambayo yanakabili mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Nchi saba za EAC zilituma wanajeshi mwishoni mwa mwaka jana katika eneo hilo. Mapigano katika jimbo la Kivu Kaskazini yamesababisha idadi kubwa ya watu kuyahama makazi yao na kuzidisha hali ya wasiwasi, huku serikali ya DRC ikiishutumu Rwanda kwa kuunga mkono M23 -- madai yaliyokanushwa na Kigali lakini yakaungwa mkono na Marekani na mataifa kadhaa ya Magharibi.
Wanamgambo hao waliibuka tena kutoka katika hali ya utulivu mwishoni mwa 2021, na baadaye kumiliki maeneo mengi ya Kivu Kaskazini, ikiwa ni pamoja na eneo kubwa la kaskazini mwa mji mkuu Goma.
EAC, ambayo imefanya mikutano kadhaa kusuluhisha mzozo huo na kutoa wito wa kuondolewa kwa M23 kutoka maeneo yaliyokaliwa, iliunda kikosi cha kikanda kinacholenga kuleta utulivu mashariki mwa DRC.
Taarifa ya EAC kwa vyombo vya habari siku ya Ijumaa ilithibitisha kuwa wanajeshi wa Burundi watatumwa, lakini haikufafanua idadi ya wanajeshi wanaosafiri kwenda DRC.
Kulingana na ratiba mpya iliyopitishwa na viongozi wa Afrika Mashariki mwezi uliopita, "makundi yote yenye silaha," ikiwa ni pamoja na M23, lazima yaondoke ifikapo Machi 30.
Katika uwanja wa ndege siku ya Jumapili, Jenerali Emmanuel Kaputa Kasenga, naibu kamanda wa kikosi cha Afrika Mashariki, alikutana na waliofika kutoka Burundi na kuzungumza juu ya dhamira yao.