Kesi hizo barani Afrika zinachangia jumla ya wanahabari 361 waliofungwa jela duniani kufikia Disemba 1, kulingana na shirika la kutetea haki za waandishi wa habari, CPJ.
Idadi hiyo ni ya pili ya juu kuwahi kurekodiwa na CPJ.
Muthoki Mumo, mratibu wa programu ya CPJ barani Afrika, alisema ripoti hiyo inaangazia mwelekeo wa kimataifa ambapo tawala za kimabavu hutumia sheria kama zana za kukandamiza wanahabari, kwa kutumia sheria za usalama wa taifa, kupambana na ugaidi na uhalifu wa mtandaoni ili kuhalalisha ukandamizaji huo.
Nchi zikiwemo Burundi, Ethiopia na Nigeria zinatumia sheria iliyowekwa kwa ajili ya usalama wa umma kufanya uandishi wa habari kuwa kosa la jinai, Mumo alisema.
Nchini Nigeria, “Kuna wanahabari wanne gerezani waliofunguliwa mashtaka chini ya sheria ya uhalifu wa mtandaoni kuhusiana na ripoti zao kuhusu ufisadi,” Mumo aliiambia VOA katika mahojiano ya Video.
Na nchini Ethiopia, waandishi sita wapo gerezani. “Watano kati yao wanakabiliwa na mashtaka chini ya sheria za kupambana na ugaidi. Wanaweza kukabiliwa na adhabu kali ikiwa watakutwa na hatia,” alisema Mumo.
Nchini Burundi, Sandra Muhoza, mwandishi wa habari wa chombo cha habari cha mtandaoni, La Nova, alihukumiwa chini ya sheria za usalama wa taifa baada ya kutuma ujumbe wa WhatsApp. Kesi hiyo, alisema Mumo, ni mfano wa wazi wa kufanya uandishi wa habari kuwa kosa la jinai.