Wanahabari 20 nchini Uganda wamepigwa na kujeruhiwa na jeshi la polisi nchini humo

Wanahabari nchini Uganda wakiwa katika majukumu yao ya kazi

Ofisi ya UN nchini Uganda imesema Ofisi ya kamisheni ya haki za binadamu ilipata waraka huo kutoka kwa kiongozi wa upinzani Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine na kwamba ofisi hiyo itaanza kuchunguza mara moja madai hayo na kuchukua hatua zinazohitajika

Maafisa wa jeshi na polisi nchini Uganda waliwapiga vibaya na kuwajeruhi waandishi wa habari waliokua wanaripoti kuhusu waraka wa maandishi juu ya vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu uliowasilishwa kwenye ofisi ya Umoja wa Mataifa.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Uganda imesema Ofisi ya kamisheni ya haki za binadamu ilipata waraka huo kutoka kwa kiongozi wa upinzani Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine na kwamba ofisi hiyo itaanza kuchunguza mara moja madai hayo na kuchukua hatua zinazohitajika. “Mwenendo huu unakiuka makubaliano na serikali, kukiangaziwa usalama wa majengo ya Umoja wa Mataifa, wafanyakazi na wageni”, ofisi ya Umoja wa Matifa imesema katika taarifa.

Polisi imesema maafisa wa usalama walitawanya umati usiodhibitiwa ambao ulikua umekusanyika nje ya ofisi ya Umoja wa Mataifa, wakati Bobi Wine akiwasilisha waraka huo.

Waandishi wa habari Uganda wakifuatilia habari nchini humo

"Kwa bahati mbaya, kuna watu wachache waliopata majeraha mkiwemo wanahabari. Tumeanzisha uchunguzi kujua ni katika mazingira gani waathirika walijeruhiwa’, polisi imesema katika taarifa.

Waandishi wa habari 20 walijeruhiwa katika shambulizi hilo, na angalau wanne walikua na majeraha makubwa kichwani, katibu mkuu wa chama cha wanahabari wa Uganda, Stephen Bwire ameliambia shirika la habari la Reuters.