Wanafunzi washinikiza bunge la Marekani kuchukua hatua

Maelfu ya wanafunzi waliojitokeza kuandamana mjini Washington, DC, Machi 14, 2018.

Maelfu ya wanafunzi nchini Marekani wametoka madarasani katikati ya vipindi vya masomo asubuhi Jumatano kulalamika juu ya hatua ya bunge la Marekani kushindwa kufanya maamuzi ya kuzuia uvunjifu wa amani unaotokana na mashambulizi ya kutumia silaha katika shule za Marekani na kuwakumbuka wale waliouwawa kwa bunduki mwezi Februari katika shule ya sekondari ya Florida.

Maandamano hayo yalidumu kwa dakika 17, kila dakika ikimwakilisha mwanafunzi mmoja kati ya 14 na watu wazima watatu wote waliuwawa katika shambulizi hilo lililotokea siku ya Wapendanao – Valentine wakati mtu mwenye umri wa miaka 19 ambaye alikuwa na matatizo aliposhambulia kwa bunduki shule ya sekondari ya Marjory Stoneman Douglas huko Parkland, Florida.

Kufikia mwezi mmoja siku ya leo tangia shambulizi hilo lilipotokea na kuleta taharuki kubwa katika muda ambao masomo yalikuwa yanafikia ukingoni, mamia ya wanafunzi walikusanyika katika uwanja wa mpira kupinga kitendo cha bunge kutochukua hatua yoyote baada ya mauaji hayo na kujikumbusha shambulizi hilo wenyewe kwa wenyewe.

Walioandaa maandamano hayo wanasema takriban wanafunzi 3,000 walipanga kutoka madarasani nchi nzima, wakati maandamano mengine yalifanyika mbele ya ikulu ya White House na Bunge la Marekani. Baadhi ya viongozi wa shule za hapa nchini wameunga mkono maandamano hayo, lakini wengine wamesema wanafunzi hao watachukuliwa hatua za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kusimamishwa masomo kwa kutoka nje ya madarasa bila ya kupewa ruhusa.

Katika baadhi ya jamii, wazazi wakiwa wamebeba mabango waliungana na watoto wao wakishinikiza sheria kali za udhibiti wa silaha kuanzishwa Marekani, ambako Katiba inaruhusu umiliki wa silaha na bunge limekuwa likipinga mapendekezo ya kuwekea mkazo sheria za kudhibiti ununuzi wa silaha.

Tawi la vijana la kikundi cha wanawake Women March Youth Empower ambalo limeandamana dhidi ya Rais Donald Trump limesema linajipanga kuandamana “ kupinga kitendo cha bunge la Marekani kutochukua hatua yoyote zaidi ya kutuma ujumbe wa tweet na maombi kufuatia shambulizi la uvunjifu wa amani kwa kutumia bunduki lililoziathiri shule zetu na wale wanaoishi katika maeneo jirani na shule hizo.”

“Wanafunzi na wafanyakazi mashuleni wanahaki kufundisha na kujifunza katika mazingira yaliyokuwa hayajagubikwa na wasiwasi wa kushambuliwa na bunduki wakiwa madarasani au wakati wanatoka shuleni kurejea majumbani mwao,” waandaaji wa maandamano hayo wamesema.

“Sisi hatuko salama tukiwa mashuleni. Hatuko salama katika miji na vitongoji vyetu. Bunge lazima lichukue hatua za kuridhisha ili kutuhakikishia usalama wetu na lipitishe mabadiliko ya sheria za silaha katika serikali kuu,” kikundi hicho kimesema.