Jumuiya ya Kimataifa Yatoa wito wa kuwepo Uchaguzi wa Amani Kenya

Kituo cha kuwaandikisha wapiga kura Kenya

Jumuiya ya Kimataifa imesema kuwa haitajihusisha na siasa za chama chochote wakati wa uchaguzi nchini Kenya.

Wakati Kenya ikijitayarisha kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2017, mabolozi wa kigeni mjini Nairobi wameahidi kusaidia Kenya kuandaa uchaguzi mkuu ambao ni huru na wa haki.

Balozi wa Finland nchini Tarja Fernández, amesema Ijumaa kuwa Kenya ina jukumu kubwa kuhakikisha kuwa uchaguzi mkuu unafanyika kwa amani.

Kwa upande wake balozi wa Denmark nchini Kenya, Mette Knudsen ameipongeza tume ya uchaguzi nchini, IEBC, kwa weledi na utaalamu wake katika zoezi la kuwaandikisha wapiga kura.

Amesema kuwa wanahitaji kuungwa mkono na wakenya na viongozi wa kisiasa katika kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani.

Kupitia mabalozi wake nchini, jumuiya hiyo pia imeahidi kuendelea kuisaidia Kenya katika kuhakikisha kuna amani wakati wa uchaguzi.

Kauli ya Mabalozi

Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA ameripoti kuwa wanadiplomasia hao walikuwa wanatembelea maeneo tofauti nchini humo kutathmini miradi inayofadhiliwa na serikali zao.

Pia wameiambia VOA kuwa wataendelea kuisaidia Kenya kuandaa uchaguzi, lakini jukumu la kuchagua viongozi wanawaachia Wakenya wenyewe.

Wanawake Wahamasishwa

Mwandishi wa VOA ameripoti kuwa wakati kukiwa na idadi ndogo ya wawanake waliochaguliwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2013, katika mabunge ya kitaifa na yale ya kaunti, mabalozi hao wamehimiza wanawake kujitokeza kwa wingi kupigania nyadhifa za kisiasa kama ilivyo katika katiba ya Kenya ya mwaka 2010.

Balozi Mette amesisitiza kuwa wanawake wasiogope kukabiliana na changamoto zilizoko katika kuwania nyadhifa za kisiasa. Amewataka wajaribu kugombea na wasitishwe na uwezo wa kifedha, bali wajitokeze na kuzinadi sera zao kwa wapiga kura.

Wakati Joto la kisiasa likionekana kupanda kote nchini aviongozi wa kisiasa wamekuwa wakishawishi wakenya kuwaunga mkono katika uchaguzi mkuu,

Mwanahawa Salim ambae ni balozi wa amani hapa Pwani , amehimiza Wakenya kujiepusha na kauli zenye chuki wakati huu ambapo taifa linaelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2017.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Amina Chombo, Kenya