Wanachama wanne wa kundi linalomuunga mkono Trump wapatikana na hatia ya kutaka kuipindua serikali

Wanachama wa kundi lenye itikadi kali ya mrengo wa kulia (Oath Keepers) wakisimama nje ya jengo la bunge la Marekani, Januari 6, 2021.

Wanachama wanne wa kundi la itikadi kali ya mrengo wa kulia hapa Marekani (Oath Keepers) Jumatatu walipatikana na hatia ya njama ya kuipindua serikali kwa kuhusika kwao katika shambulizi la Januari 6, 2021 dhidi ya Bunge la Marekani, lililofanywa na wafuasi wa rais wa zamani Donald Trump.

Uamuzi huo unaashiria mwisho wa kesi ya pili kubwa ya uchochezi dhidi ya wanachama wa kundi hilo lenye itikadi kali ya mrengo wa kulia, ambao walikuwa miongoni mwa mamia walioshambulia Bunge la Marekani katika jaribio ambalo halikufanikiwa la kulizuia Bunge kuidhinisha ushindi wa Joe Bidem dhidi ya Trump, katika uchaguzi wa rais wa 2020.

Wajumbe 12 wa jopo la wasaidizi wa mahakama wamewapata wanachama wa Oath Keepers David Moerschel, Joseph Hackett, Roberto Minuta na Edward Vallejo na hatia ya njama ya kuipindua serikali.

Wanne hao pia walipatikana na hatia ya kulizuia Bunge kuidhinisha uchaguzi wa rais wa 2020, na mashtaka mengine mawili ya njama yanayohusiana na shambulio la bunge.