Wamarekani walisheherekea sikukuu ya shukrani inayojulikana kama Thanksgiving. Siku hii husheherekewa Alhamis ya mwisho ya mwezi Novemba kila mwaka ni utamaduni wa miaka mingi kwa taifa hilo ambapo hukutanisha familia, ndugu na marafiki na kukaa wakila pamoja nyama ya bata mzinga aliyeokwa na kuandaliwa pamoja na milo midogo midogo kama vile viazi mbatata, maharage machanga, maboga na kadhalika.
Pia kunakuwepo na gwaride maalumu kwa ajili ya siku ya Thanksgiving pamoja na michezo maalumu inayohusisha watu wa rika zote. Maduka mengi hufungwa majira ya asubuhi na hufunguliwa saa za jioni huku kukiwa na punguzo kubwa la bei kwa bidhaa na kuanzia hapo huashiria mwanzo wa kununua na kutayarisha zawadi kwa ajili ya sherehe za kufunga mwaka mmoja kwenda mwaka mwingine.
Katika sherehe za mwaka huu hali ya usalama iliongezwa ikiwemo mbwa maalumu wenye uwezo wa kunusa vitu na kugundua kama kuna kitu kinachoweza kuhatarisha jamii. Idara ya polisi katika mji wa New York mahala ambapo kunafanyika gwarise la kila mwaka la Thanksgiving ilisema imeweka polisi 3,000 kuweza kulinda usalama kwenye sherehe hii.