Maafisa wa jeshi la ulinzi wa taifa, kikosi kinachotoa ulinzi wa muda kwa ajili ya usalama wa kuapishwa Rais Mteule wa Marekani Joe Biden, wanasema wameondoa walinzi 12 katika kikosi hicho ikiwa miongoni mwa hatua za kuhakikisha usalama kwenye sherehe za kuapishwa kwa Biden, Januari 20.
Ulinzi umeongezeka kufuatia vurugu zilizosababisha vifo Januari 6 baada ya jengo la bunge kushambuliwa na wafuasi wa rais anayeondoka madarakani Donald Trump.
Msemaji mkuu wa Pentagon, Jonathan Hoffman amewaambia waandishi wa habari kwamba walinzi 10 kati ya 12 waliondolewa kwa tabia inayotia shaka ambayo haihusiani na msimamo mkali ulioelezwa na FBI wakati wa ukaguzi wa walinzi wote 25,000 waliopelekwa katika eneo la Washington kwa ajili ya shughuli za kuapishwa Biden na Makamu Rais wake mteule Kamala Harris.
Wengine wawili waliondolewa kazini baada ya kutoa matamshi au maandishi yasiyofaa, Hoffman alisema bila kuelezea majina yao.