Walinda mbuga wauwawa DRC

Walinda mbuga wa mbuga ya Virunga wakishika doria

Watu wenye silaha Jumapili wameuwa walinda mbuga sita ,huku wengine wakijeruhiwa kwenye mbuga ya taifa ya wanyama ya Virunga ,mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwenye eneo maalum linalohifadhi nyani wa milimani.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, msemaji wa mbuga hiyo Olivier Mukisya amesema kuwa haijabainika waliotekeleza ukatili huo ingawa mashambulizi ya awali yamekuwa yakifanywa na wapiganaji wanaotaka udhibiti wa utajiri mkubwa wa maliaslili mashariki mwa DRC.

Zaidi ya walinda mbuga 200 wameuwawa kwenye mbuga ya Virunga wakiwemo 12waliouwawa mwezi Aprili mwaka uliopita. Mbuga ya Virunga iko kwenye misitu mikubwa katikati mwa Afrika ambako inaaminika kuwa takriban nusu ya idadi ya nyani wa milimani wanaishi.

Mbuga hiyo ndiyo ya muda mrefu zaidi barani Afrika na pia kubwa zaidi yenye misitu na mvua nyingi ikiwa na ukubwa wa kilomita 7,800 mraba. Makundi mengi ya wapiganaji yanapatikana mashariki mwa Congo, mengi yakiwa mabaki ya vita vya wenyewe kwa wenyewe mwanzoni mwa karne, vilivyouwa mamilioni ya watu.

Mtayarishi- Harrison Kamau