Walinda amani watano wa Umoja wa Afrika nchini Somalia wamekamatwa kwa shutuma za kujaribu kuuza vifaa vya kijeshi katika mji mkuu, Mogadishu.
Vikosi vya usalama vya Somalia pamoja na vikosi kutoka tume ya Umoja wa Afrika nchini Somalia-AMISOM walisema wamefanya uvamizi kwenye garaji moja ambapo wanajeshi wa AU wanashutumiwa kujaribu kuuza vifaa vya jeshi ikiwemo masanduku ya risasi, mafuta na mifuko ya mchanga.
AMISOM haivumilii utendaji usiofuata maadili ya kikazi miongoni mwa wafanyakazi wake na washukiwa hao watafunguliwa mashtaka kulingana na sheria, AMISOM ilisema Jumatatu.
Tume hiyo ilisema nchini Somalia ina wanajeshi 22,000 hawatayumbishwa na vitendo vya ubinafsi vya wanajeshi wake wachache. AMISOM haikutaja utaifa wa wanajeshi hao lakini iliahidi kwamba itawataja ili kuhakikisha kwamba jambo hilo halivumiliwi ndani ya jeshi lake.
Wanajeshi wa AU wanaisaidia serikali ya Somalia kupambana na uasi wa kundi la wenye msimamo mkali wa ki-Islam la al-Shabaab.