Msafara wa wanajeshi wa kikosi cha Umoja wa Mataifa wa Mali ulishambuliwa tena na vilipuzi mwishoni mwa juma, na kuwajeruhi walinda amani 22 zaidi katika harakati za kuondoka nchini humo, msemaji wake amesema Jumatatu.
Mamia ya magari ya MINUSMA yalianza safari Oktoba 31 kutoka mji wa Kidal kaskazini mashariki mwa Mali, lakini bado hawajafika Gao, mji mwingine wa muhimu wa kijeshi ulio umbali wa kilomita 350.
“Siku ya Jumamosi, msafara huo ulikumbana na vilipuzi vingine viwili karibu na mji wa Anefis,” Stephane Dujarric, msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, aliwaambia waandishi wa habari Jumatatu.
Alisema kuwa walinda amani 22 walilazimika kuhamishwa kwa ndege ili kupokea matibabu ya haraka huko Gao.
Ni tukio la sita tangu msafara huo kuondoka Kidal, Dujarric alisema, akiongeza kuwa safari zote za uokoaji za matibabu zilifanya kazi bila matatizo yoyote.