Wajumbe wa serikali na viongozi wa chama cha walimu wameshindwa kukubaliana juu ya madai ya kuajiri walimu zaidi kukidhi mahitaji ya masomo nchini Kenya.
Waziri Mkuu Raila Odinga alikutana Jumatatu na viongozi wa chama cha waalimu katika juhudi za mwisho za kujaribu kuzuia mgomo huo kuendelea, lakini walimu wanashikilia kwamba serikali inabidi kuajiri takriban walimu 19,000.
Mwandishi wa Sauti ya Amerika mjini Nairobi Mwai Gikonyo anaripoti kwamba tatizo kubwa ni kwamba fedha zilizotengwa kuwalipa walimu wapya zimetumiwa kulipa madeni ya wabunge.
Kwa upande mwingine vyanzo vya habari vinaeleza kwamba fedha hizo za walimu zimetumiwa pia kulipa nyongeza ya mishahara ya wanajeshi.
Akizungumza na Sauti ya Amerika, mwalimu wa shule ya msingi ya Nivasha, Esther Njuguna anasema tatizo kubwa ni kwamba hawana walimu wa kutosha kukabiliana na idadi kubwa ya wanafunzi. Anasema kwa wastani darasa moja lina karibu wanafunzi 100 kwa mwalimu mmoja.